Habari

Kura zinazoharibika kwenye chaguzi zinasababishwa na wapiga kura kukosa elimu ya mpiga kura.

Imewekwa: 2017-05-29 15:41:23

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema kuwa kura zinazoharibika kwenye chaguzi zinasababishwa na wapiga kura kukosa elimu ya mpiga kura.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume hiyo Bw. Kailima Ramadhani wakati akijibu swali la mmoja wa watangazaji wa kituo cha Redio AFM cha mkoani Dodoma aliyehoji kuhusu sababu za kuharibika kwa kura unapotokea uchaguzi katika mfululizo wa vipindi vya utoaji wa elimu ya mpiga kura kupitia vituo vya redio.

Bw. Kailima amesema kuwa kinachosababisha hali hiyo ni ukosefu wa elimu ya mpiga kura kwa wananchi, na ndio maana Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria ya Taifa ya Uchaguzi iliona umuhimu wa kutoa elimu hiyo katika kipindi chote cha mwaka.

Amesema kifungu cha 4C cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi kinaeleza kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi itatoa elimu ya mpiga kura na kuongeza kuwa kumekuwa na changamoto ya kutotoa elimu ya mpiga kura baada ya uchaguzi. Aidha, amesema kuwa elimu imekuwa ikitolewa wakati wa uchaguzi na baada ya uteuzi wa wagombea na wakati wa kampeni

“Kama Tume na wadau wanaanza kutoa elimu ya mpiga kura katika kipindi hicho, sasa mpiga kura atazingatia kusikiliza kampeni za chama badala ya kusikiliza utaratibu mzima wa namna ya kupiga kura kama”

Amesema Tume imeanza kutoa elimu ya mpiga kura katika kipindi chote cha mwaka hali itakayosaidia kupunguza au kuondoa kuharibika kwa Kura wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 .

“Kwa mujibu wa mwongozo na maelekezo yaliyotolewa na Tume kwa wasiamamizi wa uchaguzi, alama yoyote ikiwemo ya X itakayowekwa kwenye chumba cha picha ya mgombea au jina la chama cha mgombea au kwenye chumba cha wazi itakubalika kwamba ni alama halali” alisema.

Alifafanua kuwa karatasi ya kura itakataliwa iwapo haina muhuri wa kituo au itakuwa na kitu au alama inayomtambulisha mpiga kura na iwapo, haijawekwa alama inayotambuliwa kuwa ni halali.

Aliongeza kuwa karatasi ya kura itakayopigwa kwa mgombea aliyejitoa kwa mujibu wa Sheria za Uchaguzi au ikawekwa alama kwa mgombea zaidi ya mmoja na iwapo haina alama yoyote, itakataliwa.

Hata hivyo, Bw. Kailima aliongeza kuwa uamuzi wa uhalali wa kura kituoni utaamuliwa na msimamizi wa kituo iwapo atarijiridhisha kuwa kura imeharibika na haiwezi kuhesabiwa na ataikataa na haitahesabiwa.

Tume imeanza kutekeleza mpango wa kutoa elimu ya mpiga kura kupitia vituo vya redio za kijamii katika mikoa yote ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ikiwa ni sehemu ya kutekeleza matakwa ya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi ya kutoa elimu ya mpiga kura muda wote.