Habari

Wagombea wawili wajitoa kwenye uchaguzi mdogo wa Udiwani

Imewekwa: 2017-11-17 11:35:52


Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeridhia kujitoa kwa wagombea wawili wa Udiwani katika Kata ya Milongodi, Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba Mkoani Mtwara na Kata ya Ndalambo katika Halmashauri ya Wilaya Momba mkoani Songwe.

Wagombea waliojitoa ni Ndugu Lunda Rashid Ulaya wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutoka katika kata ya Milongodi Halmashauri ya wilaya ya Tandahimba na Juma Mohamed Siyame wa Chama cha ACT Wazalendo kutoka kata ya Ndalambo katika Halmashauri ya Momba.

Katika kikao cha chake kilichofanyika tarehe 14/11/2017 jijini Dar es Salaam, Tume imeridhia uamuzi wa kujiondoa kwa wagombea hao wawili katika nafasi ya udiwani, baada ya kukamilisha taratibu zote za kujitoa.

Miongoni mwa taratibu hizo ni mgombea kuandika barua kwa msimamizi wa uchaguzi wa jimbo au msimamizi msaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata kumjulisha uamuzi wa kujitoa .

Katika barua yake kwenda kwa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Kata, mgombea wa kata ya Milongodi Ndugu Lunda Rashid Ulaya katika barua yake ya tarehe 4/11/2017 hakueleza sababu zilizomfanya ajitoe kwenye kinyanganyiro hicho cha kugombea udiwani.

Kwa upande wake mgombea wa ACT WAZALENDO Ndugu Juma Mohamed Siyame, katika barua yake ya tarehe 10/11/2017 alieleza sababu za kujitoa ni kuwa na majukumu ya kifamilia na hivyo asingeweza kumudu kuwatumikia wananchi wa Ndalambo katika shughuli mbalimbali za maendeleo.

Kutokana na kujiondoa kwa wagombea hao, idadi ya wagombea waliobaki katika kinyanganyiro hicho sasa ni 151. Uchaguzi mdogo wa madiwani unafanyika katika kata 43 ambazo ziko katika Halmashauri 36 kwenye mikoa 19 Novemba 26, 2017.