Tume ya Taifa Ya Uchaguzi

Tume ya Uchaguzi ndio inajishughulisha na maamuzi yote kuhusu Sera na mipango katika taasisi. Maamuzi na sera kuhusu utendaji wa kila siku huamuliwa na vikao vinavyoongozwa na mwenyekiti wa Tume na kama hatakuwepo Makamu Mwenyekiti ataongoza vikao.

Akidi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ni Wajumbe wanne akiwemo Mwenyekiti.  Maamuzi yote huamuliwa kwa uwingi wa Kura na Tume inaweza kuendelea na shughuli zake hata kama idadi ya Wajumbe haitatimia .Tume kwa mujibu wa Sheria za Uchaguzi inaweza kutengeneza kanuni na maelekezo yoyote yanayosimamia mchakato wa Uchaguzi.

Chini ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi yupo Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye pia huteuliwa na Rais na ambaye ndiye Afisa Mtedaji mkuu na ndiye Mkuu wa Sekretarieti.

MUDA WA UTUMISHI WA KAMISHNA WA TUME

Kamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ataacha kuwa mjumbe wa Tume baada ya kumalizika kwa muda wake wa miaka Mitano tangu ateuliwe ama kutokana na sababu nyingine zozote zitakazomfanya ashindwe kutimiza majukumu yake.

Rais anaweza kumuondoa Kamishna endapo tu atashindwa kutekeleza majukumu yake kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo la kuwa na mwenendo usiofaa.